Thursday 12 April 2012

LULU AFIKISHWA MAHAKAMANI..

Muigizaji wa Filamu nchini anaehusishwa na kifo cha Muigizaji Mwenzie,Marehemu Steven Kanumba,Bi Elizabeth Michael a.k.a Lulu amepandishwa kizimbani mapema leo asubuhi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam kwa kusomewa mashtaka yake kuhusiana na kuhusika kwa kifo cha Muigizaji huyo nguli hapa nchini.

Elizabeth Michael amesomewa mashtaka hayo mbele ya hakimu Agustino Mmbando na wakili Elizabeth Kaganda ya mauaji ya Muigizaji wa Filamu nchini,Marehemu Steven Kanumba yaliyotokea huko sinza vatcan jijini Dar es Salaam april 7 mwaka huu.

Elizabeth Hakutakiwa kujibu chochote Mahakamani hapo kwani mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji. Kesi hiyo imeahirishwa na kupangwa kusikilizwa tena april 23 mwaka huu. Muigizaji huyo aliletwa mahakamani hapo kwa mwendo wa kasi kama mshale na kwa ulinzi mkali na pia ndivyo alivyoondolewa Mahakamani hapo Kwa gari ndogo nyeupe aina ya suzuki grand vitara yenye nambari za usajiri T 848 BNV huku kwenye kioo nambari zake zikisomeka PT 2565.

BBC SWAHILI HAD THIS TO SAY;

Amefikishwa mahakamani ikiwa ni siku nne, tangu alipokamatwa mara baada ya kifo cha msanii huyo ambaye inaaminika kuwa walikuwa na uhusiano wa Kimapenzi.
Taarifa zinazohusiana
Afrika, Tanzania
Mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam,Bi Augustina Mbando,Elizabeth Michael Kimemeta ajulikanaye kama Lulu kwa jina la Usanii,aliwasili mahakamani hapo akiwa chini ya Ulinzi mkali wa askari Polisi waliokuwa wamevaa kiraia na wengine wakiwa wamejihami kwa silaha.
Mara baada ya Kufikishwa mahakamani,upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa serikali Bi Elizabeth Kaganda ulimsomea shtaka moja ambalo ni la mauaji, kosa ambalo ni kinyume cha sheria ya kanuni ya adhabu kifungu cha 196.

Wakili huyo wa serikali Bi Elizabeth Kaganda,alidai mbele ya mahakama kuwa mnamo tarehe 07 mwezi April mwaka 2012,katika eneo la Sinza Vatican,msanii Elizabeth alimuua msanii Steven Kanumba.

Akiwa amevalia gauni kubwa lijulikanalo kama dera lenye rangi ya Njano mtandio wa rangi ya waridi na kandambili nyekundu mshtakiwa alionekana kutokuwa na wasi wasi pamoja uzito wa tuhuma za mauaji anayokabiliwa nayo huku akijibu maswali kadhaa kuhusu wasifu wake.
Msanii huyo alikanusha kuwa na umri wa miaka 18 baada ya kuulizwa ,ambapo yeye amesisitiza kuwa ana umri wa miaka 17, hii ikiwa ni tofauti na habari ambazo zimekuwa zikiripotiwa kuhusu umri wa msanii huyo ambaye sasa anatambulika kama mshtakiwa.
Kesi hii ya mauaji inatajwa kwa mara ya kwanza na mshtakiwa hakutakiwa kukiri wala kukana mashtaka.
Upande wa mashtaka umeieleza mahakama kuwa kesi bado iko kwenye upelelezi ambapo inatarajiwa kutajwa tena April 23 mwaka huu.
Mshtakiwa amepelekwa rumande hadi siku hiyo wakati kesi hii itakapotajwa tena.
Kwa upande mwingine tukio la kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo kumefanywa kwa usiri mkubwa na kufanya waandishi wa habari wengi wameshindwa kufuatilia kwa karibu tukio lenyewe.
Kufikishwa mahakamani kwa msanii huyo na kusomewa shtaka la mauaji ya Kanumba kumetokea siku moja baada na Marehemu Steven Kanumba kuzikwa katika makaburi ya Kinondoni.
Mazishi yake yalichukua sura ya kitaifa kutokana na umaarufu aliojijengea msani huyo katika jamii ya watanzania na hata nchi za nje

No comments: